HISTORIA

HISTORIA YA HUDUMA YA THE OASIS OF HEALING MINISTRIES

Mchungaji Prosper na Deborah Ntepa ndio waanzilishi wa huduma ya The Oasis of Healing Ministries (OHM). Kati ya Septemba 1996 na Novemba 2005, walianza kwa kufanya kazi chini ya Askofu Bernard Nwaka chini ya mwamvuli wa Restoration Bible Church kwa miaka tisa kabla hawajaanzisha huduma yao wenyewe. Kwanza walianzisha kanisa pale Mnazi Mmoja mjini Dar es Salaam chini ya Restoration Bible Church tarehe 29 Septemba 1996, kanisa ambalo lilianza kugusa mamia ya watu kupitia mafundisho, uponyaji na kufunguliwa. Kanisa hili lilizaa makanisa mengine huko Kigamboni, Tandika, Kawe, Moshi na Morogoro. Prosper na Deborah Ntepa walifanya kazi chini ya mwamvuli wa Restoration Bible Church kwa miaka 9 mpaka tarehe 20 Novemba 2005 wakati Mungu alipowapa mwelekeo mpya. Mchungaji Prosper Ntepa na Deborah Ntepa walioana tarehe 15 Oktoba 1988. Wamebarikiwa kwa kupata mabinti wanne: Alice, Angela, Faraja na Shaddai.

Mke wa Mchungaji Prosper pia ni mchungaji aliyesimikwa. Hapo mwanzoni alikuwa anaitwa Rhoida. Mwaka 2005 alibadilisha jina lake kwa kutii neno la kinabii alilolipokea Juni 2002 toka kwa Mtume Greg Howse. Mtume Prosper na Deborah Ntepa wamekuwa wakihudumu pamoja katika sehemu mbalimbali duniani. Deborah Ntepa ameandika vitabu 12 ikiwa ni pamoja na hivi: Usikate Tamaa Muujiza Wako Uko Njiani, Utasa Unaponyeka, Unaweza Kumsikia Mungu, Jinsi ya Kupata Kibali, Uponyaji wa Moyo Ulioumizwa, Jinsi ya Kujiandaa Kuolewa.

Mwezi Februari 2004, Mungu alianza kuongea na Prosper Ntepa kuhusu kuanzisha huduma ya kimataifa iitwayo The Oasis of Healing Ministries (OHM). Akamwambia kiongozi wake wakati huo Askofu Bernard Nwaka kuhusu maono yake lakini akashauriwa asubiri hadi wakati sahihi wa kuanza huduma yake.

Kwa mara nyingine mwezi Oktoba 2005, Roho Mtakatifu akaongea na Mtume Ntepa na kumwambia kwamba wakati wa kufanya kazi chini ya Askofu Nwaka ulikuwa unakaribia kwisha. Hapo tena akamweleza Askofu Nwaka kuhusu mwelekeo huo mpya. Mwishowe Askofu Nwaka akawa tayari kumwachilia. Ndipo tarehe 20 Novemba 2005, Mchungaji Prosper na Deborah wakaombewa na kuachiliwa rasmi waondoke Restoration Bible Church mbele ya mitume wafuatao: Chabbs Sibale, Stanley Mwangonde, Collins Sapalo na Israel Wandamba; na mbele ya wachungaji na waamini wa Restoration Bible Church. Waliliacha jengo la kanisa na mali nyingine zisizohamishika na kuanzisha The Oasis of Healing Ministries (OHM), ambayo ni huduma ya kimataifa na isiyofungamana na dhehebu lolote.

Kusudi la msingi la OHM si kuunda dhehebu jipya bali ni kuwafikia wale ambao hawajaokoka na pia kuufikia Mwili wa Kristo. OHM huwafundisha waamini kufanya kazi za Yesu kama vile kuponya wagonjwa, kutoa pepo, kuwapa watu wenye mahitaji mbalimbali ushauri na pia kufanya miujiza. Pamoja na hayo, huduma hii imekusudia kuwaandaa waamini kutambua karama na huduma zao na kuwatia moyo watumike badala ya kushikilia vyeo vya kimadhehebu. Msisitizo mwingine wa OHM ni ule wa kuchochea karama zile tisa za Roho Mtakatifu katika maisha ya mwamini. Pia OHM ina mpango wa kupanda makanisa kwa kadri Bwana atakavyotuongoza.

Advertisements

Powered by WordPress.com.

Up ↑

%d bloggers like this: