CHUO CHA BIBLIA

THE OASIS OF HEALING BIBLE COLLEGE (OHBC)

OHBC pamekuwa ni mahali pa mafunzo kwa watumishi lakini pia mahali pangu pa mafunzo ya kuandika vitabu kwa ajili ya uponyaji, kufunguliwa, Roho Mtakatifu, ushauri, imani na mafanikio. Shule hii ya Biblia imenisaidia kufanya utafiti kuhusiana na siri za kukufanya uweze kufanikiwa katika huduma na wito wako na kwa nini baadhi ya watumishi hushindwa katika huduma.

Chuo cha The Oasis of Healing Bible College (OHBC) ni chuo cha kipekee cha Kipentekoste kinachoweka uwiano kati ya msisitizo wa kitheolojia na ule wa matendo kwa wanafunzi katika maandalizi yao kwa ajili ya huduma. Wanafunzi wanapaswa wawe wameokoka na kujazwa Roho Mtakatifu.  OHBC hutoa mafunzo ya Diploma ya theolojia kwa muda wa miaka miwili. Kuna jumla ya masomo 50 tofauti ambayo hufundishwa kwa Kiingereza kumsaidia mwanafunzi aweze kuwasiliana vizuri katika lugha hiyo si ndani ya Tanzania tu bali pia kimataifa. Masomo hayo 50 hutolewa katika mihula 6 kwa muda wa kipindi cha miaka miwili. Kuna zaidi ya masaa 120 ya masomo (credit hours) ambayo hukamilishwa katika kozi ya Diploma wakati ambapo mafunzo ya cheti hukamilishwa kwa masaa 60 ya masomo (credit hours). Wahadhiri wa chuo hiki wana upeo mpana wa uzoefu katika huduma zilizothibitika ambazo zimeleta mabadiliko kwa watu wengi. Kwa sasa hivi, chuo hakitoi huduma ya malazi kwa wanafunzi wake lakini kuna mipango ya kujenga Shule ya Biblia katika kiwanja chetu kilichopo Kerege Bagamoyo. Kwa hiyo katika muhula wa kwanza, kozi ya Kiingereza itakuwa ni ya lazima kwa kila mwanafunzi ili waweze kuboresha uelewa wa lugha hiyo katika kuongea na kuandika pia. Kutakuwa na fursa nyingine kwa wanafunzi kufundishwa Kiingereza wakati kozi ya masomo mbalimbali ikiendelea.

 

Kwa kawaida mwaka wa masomo huanzia wiki ya kwanza ya mwezi Januari ikiambatana na kozi fupi na nzito ya Kiingereza kwa wiki moja. Katika muhula wa kwanza tutakuwa na masomo yafuatayo: Kiingereza, Kitabu cha Warumi, Manabii Wakuu (Major Prophets), Funguo za Imani Yenye Uwiano (Keys to Balanced Faith), Masomo ya Awali ya Kompyuta (Introduction to Computer –Microsoft Word, how to access the internet), Kuuelewa Upako (Understanding the Anointing), Maelekezo na Uongozi (Mentoring and Leadership). Vipindi/Mafunzo huanza saa 2.00 asubuhi hadi saa 7:20 mchana Jumatatu hadi Ijumaa.

MWANZILISHI WA OHBC:

Mtume Prosper K. Ntepa ndiye mwanzilishi wa chuo cha OHBC. Chuo cha The Oasis of Healing Bible College kilianza mafunzo yake mwezi Januari 2003 kikiwa na wanafunzi 14. Mwezi Desemba 2004, wanafunzi 3 walifanikiwa kuhitimu. Hapo awali kiliitwa Restoration International Bible College (RIBC). Mpaka sasa kimefundisha wanafunzi wanaokaribia 100.

ADA YA SHULE: Ada ya shule kwa kila muhula ni Tsh.150,000. Kwa hiyo jumla ya ada ya mwaka mzima wa masomo ni Tsh.450,000  kwa mihula mitatu (Tsh.150,000 x mihula 3). Ada zinaweza kulipwa kwa mkupuo ama kwa awamu kwa kila muhula. Ada ya muhula inapaswa kulipwa kabla kozi haijaanza. Ada ya kujiandikisha ni Tsh.10,000 na inapaswa kulipwa kabla mwanafunzi mtarajiwa hajajaza fomu ya kujiunga na chuo. Mwanafunzi atapaswa kuhudhuria masomo kwa miaka miwili ili aweze kutunukiwa Stashahada (Diploma) ya Theolojia. Mwanafunzi ambaye atahudhuria mafunzo/kozi kwa mwaka mmoja mzima atatunukiwa cheti.

FAIDA ZA KUSOMA OHBC.

Kwanza, OHBC huwaandaa wanafunzi kwa ajili ya huduma. Kumbuka kwamba kila anayeitwa na Mungu huandaliwa na Mungu na kufundishwa. Utaandaliwa ili uwe mahiri katika kile ambacho Mungu amekuitia kukifanya. Maisha yako na huduma yako hayatabaki kama yalivyokuwa baada ya kumaliza mafunzo ya miaka miwili hapa OHBC. Utaandaliwa kutimiza kusudi lako la Kimungu na wito wako.

Pili, chuo kimekusudia kuwasaidia wanafunzi kuboresha lugha yao ya Kiingereza ili kwamba waweze kusoma na kuandika vizuri kwa Kiingereza kizuri. Na matokeo yake, wahadhiri watakuwa wakifundisha kwa Kiingereza kwa wakati mwingine kusisitiza kwa Kiswahili kwa kusudi la kuhakikisha kwamba kuna uelewa wa kutosha miongoni mwa wanafunzi. Pamoja na hayo OHBC imekusudia kuwasaidia wanafunzi waweze kuhubiri kwa Kiingereza sio hapa Tanzania tu bali pia katika nchi nyingine duniani pasipo shida yoyote. Kutokana na uzoefu wetu, tumegundua kwamba vitabu vingi vizuri vya Kikristo vimeandikwa kwa lugha ya Kiingereza. Kwa sababu hiyo mtumishi wa Mungu anapaswa kuwa na uelewa mzuri wa lugha ya Kiingereza ili aweze kuwa na ufanisi katika shughuli zake za kila siku.

Tatu, chuo kimekusudia kutoa maarifa ya kiutendaji ambayo yatakusaidia kuwa mahiri katika wito wako na huduma. Chuo kinatoa masomo kama vile Siri ya Kuwa na Huduma na Wito Wenye Mafanikio (Keys to Successful Ministry and Calling), Huduma ya Uponyaji wa kiungu, Maisha ya Imani Yenye Uwiano (Balanced Faith Life), Mafanikio Yenye Uwiano (Balanced Prosperity), Upandaji wa Makanisa (Church Planting) na Kukua Kwa Kanisa (Church Growth), n.k. E.W. Kenyon anatoa ushauri katika kitabu chake kiitwacho, The Hidden Man (Mtu wa Ndani), “Nakumbuka wakati ambapo 80% ya kozi ya theolojia ilikuwa ni elimu isiyo na matumizi katika huduma ya kila siku. Hii ilionyesha ukosefu wa hekima kwa upande wa wahadhiri. Ilipaswa kuwa 80% elimu yenye matumizi ya kimatendo na 20% elimu isiyotumika. Ni ukweli unaojulikana kwamba 80% ya elimu ambayo inakusanywa mashuleni na vyuoni, kwa kusoma na kuangalia, haitumiwi na mtu wa kawaida. Hatutumii zaidi ya 10% ya uwezo na maarifa tuliyo nayo” (ukurasa 138).

Kwa sababu ya ukweli huu tumedhamiria kuweka uwiano kati ya maarifa unayohitaji kuyatumia katika huduma na maarifa ya kitheolojia ambayo hutayatumia ambayo yatatumika kama hazina kwako katika kuelewa na kutafsiri Maandiko.

Nne, OHBC inatoa maarifa ya kitheolojia ambayo yatakufanya wewe uwe na uwiano sahihi kimafundisho katika huduma yako na kufundisha. Tunatoa masomo kama vile Theology I, II na III kuwapa wanafunzi upeo mkubwa kuhusu Mungu, siku za mwisho, mafundisho kuhusu Maandiko, mafundisho kuhusu Kanisa (ecclesiology), mafundisho kuhusu malaika (angelology), mafundisho kuhusu siku za mwisho (eschatology) na mengineyo.

Tano, huduma inahitaji uelewa na maarifa mapana. Katika huduma unayokwenda kuifanya katika Mwili wa Kristo utakutana na changamoto nyingi ambazo zitayapima maarifa yako. Kwa mfano, mchungaji atahitajika kuwasaidia Wakristo katika mahitaji mbalimbali ambayo yatahitaji uelewa mpana wa Neno la Mungu na pia elimu ya kawaida ya maisha ya kila siku. OHBC itakuandaa katika huduma ya ushauri na maombezi kwa wale wenye mahitaji mbalimbali. Mtumishi wa Mungu anapaswa kuwa na maarifa. Watu watakuja kwako wakiwa na mahitaji mbalimbali.

Sita, utaandaliwa kuweza kufanya ushauri, maombi ya kuwafungua wale walioko katika vifungo vya kipepo na kuponya wale walio wagonjwa. Katika mtaala pia yamejumuishwa masomo kama vile ushauri wa kichungaji na maombi ya kufunguliwa, huduma ya uponyaji, nk. ambayo inafanikisha huduma hii. Baadhi ya matatizo utakayofundishwa katika kutoa ushauri ni pamoja na matatizo ya ndoa, ushauri kwa wanaojiandaa kuingia katika ndoa, kuwasaidia watu kuchagua kazi inayowafaa, matatizo katika mahusiano, vifungo vya ulevi, magonjwa yasiyotibika kama vile UKIMWI, vifungo vya kipepo, uzazi wa mpango, jinsi ya kuchagua mwenzi sahihi, nk.

Saba, Shule ya Biblia itakusaidia kuboresha uwezo wako wa kuyaelewa maandiko, kuyatafsiri na ujuzi wako katika kuhubiri. Utakutana na uchambuzi wa kujua maana ya asili (exegetic) wa Neno la Mungu kwa kusoma baadhi ya vitabu vya Biblia kama vile Warumi, Mwanzo, Ufunuo, Danieli, 1 Timotheo, Tito, n.k, mstari kwa mstari. Pia utasoma Mapitio ya Agano la Kale na Mapitio ya Agano Jipya (Old Testament Survey & New Testament Survey) kukupa mtazamo wa jumla wa vitabu 66 vya Biblia. Zaidi ya hayo mafundisho kuhusu ujuzi wa kutafsiri Maandiko (hermeneutics) na ujuzi wa kuhubiri (homiletics) yatawavutia sana wanafunzi.

Nane, kozi ya Stashahada (Diploma) itakujengea utamaduni wa kusoma vitabu mbalimbali. Watu wengi hawana tabia ya kusoma vitabu, licha ya tabia ya kununua vitabu. Matokeo yake, wanakosa manufaa mbalimbali ambayo wangeyapata kwa kusoma vitabu.

Tisa, utasoma kuhusu siri za mafanikio katika huduma. Utajifunza umuhimu wa tabia njema kama kigezo cha kudumisha huduma yako. Zaidi ya hayo utajifunza jinsi ya kujua kusudi lako la Kimungu na karama ama kipawa chako. Utajifunza siri ya upako na jinsi ya kuachilia upako katika maisha yako.

Kwa kweli kuna faida nyingi za kuhudhuria OHBC. Faida hizo zilizotajwa hapo juu ni baadhi tu ya zile utakazozipata ukiwa hapo. Jiandae kwa ajili ya muda mzuri utakaoutumia kuwepo katika chuo hiki. Kwa kweli maisha yako na huduma havitabaki kama ulivyokuwa huko nyuma.  Maandalizi kwa ajili ya huduma ni ya muhimu kuliko huduma yenyewe kwa sababu baada ya maandalizi ndipo unapoweza kufanya kwa ufanisi yale unayohitajika kufanya! Tunaona mambo matatu kwa wanafunzi wa Yesu Kristo. “Akapanda mlimani, akawaita aliowataka mwenyewe; wakamwendea. 14 Akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri, 15 tena wawe na amri ya kutoa pepo” (Marko 3:13-15). Kwanza, tunajifunza kwamba Yesu aliwaita wanafunzi wake. Pili, tunajifunza kwamba wanafunzi waliandaliwa kwa ajili ya huduma kwa kukaa na Yesu aliye Neno. Walikuwa pamoja na Yesu kwa takribani miaka mitatu na nusu. Walikuwa chini ya Shule ya Biblia ya Neno ya Yesu inayotembea. Tatu, wanafunzi walitumwa kwenda kuhubiri na kuzifanya kazi za Yesu kama vile kuponya wagonjwa, kutoa pepo na kutenda miujiza.

KWA MAWASILIANO ZAIDI:
Apostle Prosper K. Ntepa
P.O Box 72635
Dar es Salaam, Tanzania
Tel: +255 713 212440
                767 212440
                783 212440
Email: prosperkasesela@gmail.com
Advertisements

Powered by WordPress.com.

Up ↑

%d bloggers like this: