JINSI YA KUPOKEA UPONYAJI WA “MOYO ULIOUMIZWA” na mch. DEBORAH NTEPA

JINSI YA KUPOKEA UPONYAJI WA “MOYO ULIOUMIZWA”:

Ikiwa umeshindwa kuulinda moyo wako kwa sababu ya kuzidiwa na mambo magumu na mabaya sana; usikate tamaa, bado tumaini lipo. Wengi hudhani kwamba upako wa Roho Mtakatifu ni kwa ajili ya kuhubiri habari njema na kuombea wagonjwa tu. Lakini Neno la Mungu linaonyesha wazi kwamba kuna upako wa kuganga mioyo iliyovunjika. Isaya 61:1 inasema, “Roho ya Bwana Mungu i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo. Lipo tumaini la kupata uponyaji wa moyo uliovunjika. Kama Neno la Mungu linavyosema. Upo upako wa kuganga moyo uliovunjika. Uponyaji wa moyo ulioumizwa huambatana na uponyaji wa magonjwa yanayotokana na kuumizwa moyo. Njia zifuatazo zinaweza kukusaidia kupata uponyaji wa moyo wako

1. Kumwomba Mungu

Kama vile mgonjwa anavyomwomba Mungu kwa ajili ya uponyaji wa magonjwa, ndivyo unaweza kumwomba Mungu akuponye moyo wako. Kuna upako maalum wa kuponya mioyo iliyoumia. Haijalishi umeumizwa kiasi gani, Mungu ana uwezo wa kukuponya. Zaburi 147:3 inasema, “Huwaponya waliopondeka moyo na kuziganga jeraha zao.”

Jitahidi upate muda wa kutulia mbele za Mungu katika kuomba na kufunga. Hakika Mungu ni mwaminifu atakuponya moyo wako na magonjwa yanayotokana na kuumizwa moyo.  Zaburi 34:15, 18, 19 inasema, “Macho ya BWANA huwaelekea wenye haki, na masikio yake hukielekea kilio chao. 18 BWANA yu karibu nao waliovunjika moyo na waliopondeka roho huwaokoa. 19 Mateso ya mwenye haki ni mengi, lakini BWANA humponya  nayo yote.”

2. Kufanyiwa Ushauri na Maombezi

Unaweza kupokea uponyaji wa moyo kwa njia ya ushauri na maombezi. Kupitia ushauri unaweza kufanyiwa maombi ya kufunguliwa kutokana na pepo wa uchungu na kutokusamehe. Yakobo 5:16 inasema,“Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi na kuombeana mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana akiomba kwa bidii.” Usifiche uchungu moyoni mwako. Kwa maana ukificha uchungu moyoni utapata magonjwa. Hakikisha unashughulikia machungu yaliyo moyoni mwako. Mithali 28:13 inasema, “Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.”

3. Kunena kwa Lugha kwa Muda Mrefu

1 Wakorintho14:4 inasema, “Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake.” Mambo mengine tunayoyapitia hudhoofisha mioyo au roho zetu. Kwa njia ya kunena kwa lugha, roho yako inaweza kupokea nguvu mpya kutoka kwa mungu.

Lakini inategemea ni kwa muda gani unaokaa  kwenye maombi ya kunena kwa lugha. Mfano wa kujijenga nafsi ni kuchaji simu. Mtu anayechaji simu kwa dakika mbili ni lazima simu itaanza kuzimika baada ya muda mfupi tu. Lakini mtu anayechaji simu yake kwa muda mrefu kama masaa matatu simu yake itakuwa na nguvu ya kutumika kwa muda mrefu bila kuzimika.  Je wewe unatumia muda gani kujichaji kiroho? Ukijichaji kiroho kwa muda mfupi, ni rahisi kuishiwa nguvu za kiroho. Unapokuwa na nguvu kidogo inakuwa vigumu kustahimili mawimbi ya kiroho, hivyo inakuwa rahisi kuumizwa moyo.  Jizoeze kunena kwa lugha kwa muda mrefu. Hata kama ulikuwa umeumizwa moyo, Roho Mtakatifu atakuhuisha na kukupa nguvu za kuyaachilia yale yaliyokuumiza moyo.

4. Kutafakari na kukiri Neno la Mungu

tumia muda mwingi ukitafakari na kulitamka Neno la Mungu. Mithali 16:24 inasema, “Maneno yapendezayo ni kama sega la asali; ni tamu nafsini, na afya mifupani.” Unapokiri na kutafakari Neno la Mungu, moja kwa moja mifupa yako hupata dawa. Kwa maana maneno yapendezayo ni afya mifupani.

Pia kuna ahadi ya Mungu ya kukuondolea yasiyofaa moyoni mwako na kukupa furaha iliyo kamilifu. Isaya 61:3 inasema, “Kuwaagizia hao waliao katika Sayuni wapewe taji ya maua badala ya majivu, mafuta ya furaha badala ya maombolezo, na vazi la sifa badala ya roho nzito.” Tafakari jinsi Bwana alivyokuandalia taji ya maua, yaani kibali badala ya kukataliwa. Bwana atakupa furaha itakayobubujika toka kwenye vilindi vya moyo. Badala ya kuwa mtu wa huzuni atakuvika vazi la sifa, nyimbo zitabubujika toka moyoni mwako. Jitamkie kibali, jitamkie mafuta ya furaha, jitamkie vazi la sifa. Kwa maana Mithali 15:4 inasema, “Ulimi safi ni mti wa uzima; bali ukorofi wa ulimi huvunja moyo.”

5. Tumia Muda Wako Kukamilisha Malengo Yako

Usipoteze muda wako kwa kukata tamaa na kusononeka. Badala yake tumia muda wako kukamilisha malengo ambayo umejiwekea katika maisha yako. Usimpe ibilisi nafasi ya kuvuruga malengo yako. Nia ya Ibilisi ni kutaka kukukatisha tamaa ili ushindwe kufanikisha malengo yako. Hakikisha unampinga na kuendelea na mpangilio wa shughuli zako kana kwamba hakuna kilichotokea.

Kwa muda mrefu nilipitia mambo magumu ambayo yaliniumiza sana moyo wangu. Kuna watu ambao shetani aliwainua ili kuharibu kusudi la Mungu katika maisha yangu. Kwa muda mrefu nikawa najitahidi kuwasamehe na kuanza kufanya kazi ya Mungu. Mara nilipopata mpenyo waliinuka na jambo jingine la kuniumiza zaidi. Ndipo mtumishi wa Mungu kutoka Marekani mtume Greg Howse akanitolea unabii kwamba, “Mungu anasema, nakuponya moyo wako, nakuponya hisia zako kwa maana watu wengi wamekunenea maneno ya kukuumiza moyo wako. Nitakufanya mwanamke mwenye afya, nitakufanya mtumishi mkubwa na upako wa Deborah utakuwa juu yako.” Pamoja na kwamba shetani aliendelea kuwatumia watu wengine kunisema vibaya na kunisingizia kila neno baya, niliamua kuchukua hatua ya kukubaliana na wazo la Mungu juu ya maisha yangu.

Hakika Bwana aliuponya moyo wangu. Nikasamehe kabisa!! Kisha nikaamua kutoyaangalia mambo ambayo shetani aliyatumia kunivuruga kwa kuwatumia wale watu. Badala yake nikaamua kufanya bidii kutenda yale niliyoitiwa.

Kama ningeyaangalia mapito yangu, nisingefanyika baraka kwenye Mwili wa Kristo. Uvumilivu ni tunda la Roho ambalo kila Mkristo anapaswa kuwa nalo. Uvumilivu ni kuendelea mbele bila kubadilika hata kama unapitia mambo magumu. Uvumilivu ni sifa ya mtu anayempenda na kumcha Mungu. Katika uvumilivu mwingi Mungu amenifundisha siri ya kulinda moyo na kupokea uponyaji wa moyo.

6. Kuwekewa Mikono

Bwana alinifunulia juu ya upako wa kuganga mioyo iliyoumia kama tunavyosoma katika Isaya 61:1 inasema, “Roho ya Bwana Mungu i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo.” Ndipo nilipojifunza kuachilia upako huo kwa watu waliovunjika mioyo yao. Upako wa Roho Mtakatifu sio wa kuhubiri na kuponya magonjwa tu; bali ni pamoja na kuganga mioyo iliyoumizwa. Kwa hiyo unaweza kuwekewa mikono na watumishi wa Mungu kama vile unavyoweza kuwekewa mikono wakati unapoumwa.

7. Kusamehe na Kuchukuliana

Chanzo kikubwa cha kuumizwa moyo ni kushindwa kusamehe. Kusamehe ni msingi wa maisha ya kila Mkristo. Kwa maana mtu akishindwa kusamehe, anatembea nje ya Neno la Mungu. Baada ya kushindwa kusamehe, uchungu wa moyoni huufanya mwili kuzalisha kemikali ambazo huleta madhara katika mwili. Mithali 11:17 inasema, “Mwenye rehema huitendea mema nafsi yake; aliye mkali hujisumbua mwili wake.” Kwa faida ya roho yako na mwili wako inakupasa kusamehe. Kusamehe ni uamuzi, ukiamua kusamehe itakuwa rahisi kuondoa uchungu moyoni. Lakini usiposamehe ni rahisi kuingiwa na mapepo ya uchungu ambayo yatakufanya ujisikie uchungu zaidi. Mapepo ya uchungu huambatana na mapepo ya udhaifu ambayo hushambulia mwili. Watu wengi waliookoka hufungulia milango ya mapepo ya uchungu na mapepo ya udhaifu. Mapepo hayawezi kumwingia mtu aliyeokoka bila sababu. Mithali 26:2 inasema, “Kama shomoro katika kutangatanga kwake, na kama mbayuwayu katika kuruka kwake; kadhalika laana isiyo na sababu haimpigi mtu.” Hata kama umeonewa, inakupasa usamehe kwa ajili ya usalama wako kiroho na kimwili. Ninajua kwamba wapo watu wasiotaka suluhu kiasi kwamba hata kama wamekosa hawaoni sababu ya kutubu. Lakini unapaswa kuamua kumsamehe mtu wa jinsi hiyo kwa maana ndiyo mapenzi ya Mungu na afya ya mwili wako. Fanya jitihada ya kutengeneza na wale wote ambao hamkuelewana. Pia ujifunze kuchukuliana na mapungufu ya watu wengine.

8. Kusifu na kuabudu

Kumsifu Mungu kwa kumaanisha na kumwabudu Mungu katika roho na kweli yaani unapoabudu kwa kumaanisha kama vile uko kwenye maombi ya ndani huondoa uchungu moyoni na kuleta furaha ya Roho Mtakatifu. Watu wengi hawajihusishi na kusifu na kuabudu kwa kudhani kwamba huo ni wajibu wa waimbaji. Waimbaji ambao husimama mbele ni viongozi wa kukusaidia wewe ili uweze kusifu na kuabudu inavyokupasa. 2 Wafalme 6:14 inasema, “Daudi akacheza mbele za BWANA kwa nguvu zake zote; na Daudi alikuwa amevaa naivera ya kitani.” Mfalme Daudi alicheza mbele za BWANA akijua kuwa BWANA ndiye Mfalme mkuu. Ukilitambua hili utamsifu Mungu kwa nguvu zako zote na kumwabudu kwa moyo wako wote. Watu wengi hupokea uponyaji wa mioyo na miili yao kwa njia ya kusifu na kuabudu.

 

NB: KUFAHAMU ZAIDI JUU YA SOMO HILI TUNASHAURI UNUNUE KITABU CHA UPONYAJI WA MOYO ULIOUMIZWA KILICHOANZDIKWA NA MCHUNGAJI DEBORAH kwa kufika kanisani UBUNGO, Nyuma ya Ubungo plaza au kupiga simu namba 0715029602.

Barikiwa…

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

Powered by WordPress.com.

Up ↑

%d bloggers like this: